Katibu Mkuu Mambo Ya Ndani Ya Nchi Afanya Ziara NIDA........, Atoa Habari Njema Kwa Watumishi 597 Walioachishwa Kazi

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira amesema fedha za kuwalipa watumishi 597 waliositishiwa mikataba yao katika Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) zipo na watalipwa hivi karibuni.

Rwegasira alisema kiasi cha shilingi bilioni 2.3 zimetengwa kwa ajili ya malipo ya Watumishi hao waliaochishwa kazi Machi 7, 2016 ambapo wanaidai Mamlaka mishahara ya miezi mitatu nyuma, malimbikizo ya fedha katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na makato ya fedha za Bima ya Afya.

Akuzungumza na watumishi wa Makao Makuu ya NIDA pamoja na Maafisa Wasajili wa Vitambulisho vya Taifa, jijini Dar es Salaam jana, Rwegasira aliwataka watumishi hao waliositishiwa mikataba yao, wasipotoshwe na mtu yeyote kuhusu kutokulipwa haki zao kwani wapo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha taratibu ndogo ndogo kabla ya kuanza kuwalipa.

“Naomba muwaambie waondoe wasiwasi wowote, waache maneno, watulie kwani Serikali ipo makini na fedha tunazo na tutaanza kuwalipa mara tumalizapo taratibu ndogo ndogo zilizobaki.” Alisema Rwegasira.

Aidha, Rwegasira aliwataka watumishi wa Mamlaka hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha ifikapo Desemba 31 mwaka huu Watanzania Milioni 23 wanatakiwa watambuliwe na kupata namba kabla ya kuanza kupewa Vitambulisho vya Taifa.

Hata hivyo, watumishi hao walimuakikishia Katibu Mkuu huyo, kuwa kazi hiyo ya utambuzi itakamilika kama ilivyopangwa na itafanyika kwa umakini mkubwa kama inavyotarajiwa.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa NIDA, Dk. Modestus Kipilimba alimshukuru Katibu Mkuu huyo kwa kuwatembelea na kuwatia hamasa katika kukamilisha kazi pamoja na kufikisha lengo lao la kukamilisha utambuzi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

“Tunakuahidi Katibu Mkuu kuwa tutatimiza lengo letu na tunakuakikishia tutafanya kazi kadiri ya uwezo wetu tukiongozwa na kauli mbiu ya ‘hapa kazi tu’", alisema Dk. Kipilimba.

Katibu Mkuu Rwegasira alifanya ziara hiyo kwa lengo la kujifunza zaidi shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka, hata hivyo alipata muda wa kuzungumza na watumishi wa Mamlaka hiyo kuhusu masuala mbalimbali ya kiutendaji.

Afisa Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Ansigar Chilemba akitoa maelezo jinsi taarifa za muombaji wa Kitambulisho cha Taifa zinavyohakikiwa, kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira (kulia). Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dk. Modestus Kipilimba. Rwegasira alifanya ziara ya kikazi katika ofisi za Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam jana.



Afisa Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Ansigar Chilemba akitoa maelezo jinsi taarifa za muombaji wa Kitambulisho cha Taifa zinavyohakikiwa, kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira (kulia). Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dk. Modestus Kipilimba. Rwegasira alifanya ziara ya kikazi katika ofisi za Mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam jana.
Katibu Mkuu Mambo Ya Ndani Ya Nchi Afanya Ziara NIDA........, Atoa Habari Njema Kwa Watumishi 597 Walioachishwa Kazi Katibu Mkuu Mambo Ya Ndani Ya Nchi Afanya Ziara NIDA........, Atoa Habari Njema Kwa Watumishi 597 Walioachishwa Kazi Reviewed by on 12:28:00 AM Rating: 5