Ving’ang’anizi! Agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda la kuwataka akina dada wanaouza miili ‘makahaba’ kuondoka kwenye ‘masoko’ yao mitaani limeshindikana baada ya hivi karibuni kuonekana kwenye vijiwe vyao, Ijumaa linakupa zaidi.
Usiku wa Jumatatu na Jumanne iliyopita, makamanda wa kikosi maalum cha Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ cha Global Publishers kiliingia mitaani usiku wa saa nne kwa lengo la kuona kama madadapoa hao wamerudi baada ya kuadimika hapo kati kufuatia agizo la Makonda.
OFM ilifanikiwa kuzunguka kwenye vijiwe vya Sinza- Afrika Sana, Sinza Mori (barabara ya kuelekea Meeda Bar), maeneo ya Corner Bar, Kinondoni, Buguruni na Manzese Tip Top jijini Dar na kufanikiwa kuzungumza na baadhi yao licha ya kuwa wakali.
“Tumeamua kurudi kwa sababu ya njaa. Serikali iliposema tutoke mitaani ilitakiwa kutupeleka sehemu kufanya kazi au kutupa mitaji ya kufanyia biashara.
“Kitendo cha kuambiwa ondokeni tu halafu hatujui twende wapi wakati kula yetu, vaa yetu na watoto kusoma vyote vinategemea biashara hii, si sawasawa,” alisema Paulina Maute anayepiga kambi yake, Sinza Mori.
Mwanahawa Magembe, yeye anafanya biashara hiyo ya ukahaba maeneo ya Kinondoni ambapo kwa upande wake alisema kuwa, aliposikia agizo la Makonda kuwataka waondoke kwenye vijiwe vyao alikaa wiki moja nyumbani lakini sasa:
“Lakini sasa njaa kaka yangu, hakuna lingine njaa tu. Unaamka mpaka unalala bila kuingiza kitu kinywani. Nikaona cha kufia, ndiyo na mimi nikaamua kurudi.
“Lakini nimefika hapa na kukuta wenzangu wengine nao wamerudi.”
Hata hivyo, mazungumzo kati ya OFM na Mwanahawa yalikatishwa na wenzake waliokuja juu kwa OFM wakitaka hata kurusha mawe baada ya kubaini kuwa, kuna kamera kwenye mikono ya makanda hao.
“Mnajifanya watu wazuri kwetu kumbe hamna lolote. Kwendeni huko, tutawaumiza sisi,” walisikika wakisema wakati OFM wakiondoka eneo la tukio.
Habiba Iddi yeye anajiuza kando ya Barabara ya Shekilango eneo la Mapambano ambapo kwa upande wake alisema:
“Biashara ya ukahaba ni ya dunia nzima. Sasa nashangaa serikali yetu inavyotumia nguvu kubwa kutufukuza. Na wanaposema hii ni biashara haramu, uharamu wake uko wapi?
“Mi najua madawa ya kulevya ni haramu kwa sababu yanaua watu, vijana wanaharibika, wanakuwa mateja. Sasa sisi kwanza tunatumia kinga kujilinda na maradhi lakini pia tunapata kipato. Uharamu wake ni wapi sasa?” alihoji Habiba huku akiiomba OFM shilingi elfu tano ili achukue Bajaj kumpeleka kwao, Tandale, Dar akitoa sababu ya wateja kukosekana.
Juzi, OFM walimpigia simu Makonda kwa lengo la kutaka kujua msimamo wake baada ya agizo lake kuwekwa kapuni na madadapoa hao lakini simu yake iliita bila kupokelewa.
OFM wakamtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Christopher Fuime ili kusikia kauli yake kufuatia kiburi hicho cha machangudoa ambapo alisema:
“Tunaendelea kupambana kuhakikisha biashara hiyo tunaikomesha ingawa ni ngumu kufahamu kuwa wanapungua au wanaongezeka kutokana na kutokuwa na takwimu sahihi za wanawake wanaojiuza Dar.”
Makahaba Dar es Salaam Wamzidi Nguvu Paul Makonda
Reviewed by
on
6:32:00 AM
Rating: