Lema Akiwa na James ole Millya |
KAMPUNI ya Sky Group Associates inayomiliki mgodi wa tanzanite wa TanzaniteOne, imesema Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya amepotosha Bunge na umma juu ya suala zima la ununuzi wa hisa kwa kampuni hiyo.
Akichangia bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini mwishoni mwa wiki, Millya alisema Sky Group Associates iliyonunua hisa kwa Kampuni ya TanzaniteOne na kumiliki kitalu C Mirerani wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, haikufuata taratibu za ununuzi wa hisa hizo na kuwatuhumu baadhi ya mawaziri kuwa walihusika katika kupindisha taratibu.
Aliwataja mawaziri hao kuwa ni George Simbachawene na Jenista Mhagama, ambaye hata hivyo alikanusha madai hayo ; na ametaka taratibu za Kibunge zimlamzishe Millya, kukanusha au kuthibitisha madai yake.
Mbali ya hilo, mbunge huyo aliituhumu kampuni hiyo kwa kuwafukuza kazi wafanyakazi 201, bila ya kufuata utaratibu na kwamba inawanyanyasa .
Akizungumza na mwandishi wetu, Mwanasheria wa kampuni hiyo, Kisaka Mnzava alisema uongozi umesikitishwa na kauli ya Millya, kwa kusema alitoa kauli bila kufanya utafiti wa kina.
Mnzava alimtaka mbunge huyo, kujiridhisha kwa kufanya utafiti wa kina namna hisa za TanzaniteOne zilivyouzwa kwa Sky Group, inayomilikiwa na wazawa kwa asilimia 100.
Alisema wamiliki wa hisa wanajulikana na kama anahitaji kuwafahamu, anapaswa kwenda Mamlaka ya Usajili wa Leseni za Kampuni (Brela) kujiridhisha.
Alisema hakuna waziri wala kiongozi yeyote mwingine wa serikali, anayemiliki hisa katika Sky Group Associates.
Alisema kampuni imeshalipa kodi yote ya serikali, na kampuni hiyo sio ya mfukoni, kama anavyodai mbunge huyo.
Mnzava alisema shughuli za uzalishaji zinasimamiwa kikamilifu kati ya Sky Group na serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (Stamico), ambao ni wabia wa mgodi huo, na kwamba hakuna madini yanayoibwa kama mbunge huyo alivyosema.
Alisema hakuna njia ya mkato, iliyofanywa katika ununuzi wa hisa ; na hakuna waziri yeyote aliyehusika katika kusaidia kupindisha taratibu, kwani kila kitu kipo wazi.
Alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu), Jenista Mhagama hana ndugu na mtu anayefanya kazi TanzaniteOne.
Akizungumzia kufukuzwa kwa wafanyakazi 201, mwanasheria huyo alisema waliofukuzwa kazi ni wafanyakazi hatari kwa mustakabali wa kampuni, kwani ni wachochezi na wenye hila za kutaka kuihujumu kampuni hiyo ili ilete maafa.
Alisema kugoma ni kosa kisheria na kama mgomo haukufuata taratibu, sheria lazima zichukue taratibu.
TanzaniteOne Yamvaa Mbunge James Ole Millya, Yamtuhumu Kupotosha Bunge na Umma Bila Kufanya Utafiti
Reviewed by
on
10:24:00 PM
Rating: