Wabunge Waibana serikali Matukio ya Mauaji Mwanza


WAKATI matukio ya mauaji ya kikatili yakiendelea kuripotiwa kwenye maeneo mbalimbali nchini, Bunge limeitaka serikali kukomesha kadhia hiyo mara moja ili kuepusha maafa zaidi kwa watu wasio na hatia.

Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alitoa tamko hilo bungeni mjini Dodoma juzi wakati akitoa mwongozo kwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Amina Mollel.

Mbunge huyo alisimama na kuomba Mwongozo wa Spika akiitaka serikali itoe kauli kuhusu kuwapo kwa matukio ya mauaji hayo.

"Mheshimiwa Naibu Spika, nasimama kwa Kanuni ya 68(7), lakini vilevile nakuu kupitia Ibara ya 14 ya Katiba ya Tanzania ambayo inasema kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria," Amina alisema.

"Kumekuwapo na matukio yanayotokea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, hasa mikoa ya Manyara na Mara. Na hata jana (Jumatano) kulifanyika mauaji ya familia moja, baba na mama wamekatwakatwa mapanga na cha kusikitisha zaidi, huyo mama alikuwa ni mjamzito.

"Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kauli ya serikali kwa mwongozo wako wewe ili basi tupate kauli ya serikali kwa sababu mauaji haya yamekuwa yakitokea kwa watu wasiokuwa na hatia.

"Ni lini na nini wajibu wa serikali katika kuhakikisha kwamba raia wote wa Tanzania wanaishi kwa amani na utulivu?" Alihoji.

Akitoa mwongozo wake kuhusu suala hilo, Dk. Ackson alisema: "Kwanza nianze kwa kusikitika sana kwa niaba yenu waheshimiwa wabunge, haya mauaji yamekuwa yakiendelea kila wakati, lakini tutakumbuka waheshimiwa wiki hii, nadhani Jumatatu au Jumanne tulisikia kauli ya serikali kwamba wanafanya nini lakiniSASA mauaji haya yametokea tena jana kwa mujibu wa ripoti ya Mheshimiwa Amina Mollel."

"Lakini nikumbushe tu masikitiko yetu makubwa kwamba mauaji haya yanaendelea. Tunaiomba serikali, tafadhali ifuatilie kwa karibu ili mauaji yakomeshwe, lakini cha kukumbushana waheshimiwa wabunge, jambo kama hili haliombewi mwongozo,” alisema na kuongeza: “ Jambo kama hili linaletwa kwa kutumia kanuni nyingine ambayo siyo kanuni ya kuomba Mwongozo wa Spika kwa sababu Mwongozo wa Spika unaombwa kwa jambo lililotokea bungeni mapema," alisema

Mei 19, ikiwa ni siku moja baada ya kutokea kwa mauaji msikitini jijini Mwanza, Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, alisema vyombo vya ulinzi na usalama vitafuatilia kwa kina chanzo cha matukio hayo nchini.
Wabunge Waibana serikali Matukio ya Mauaji Mwanza Wabunge Waibana serikali Matukio ya Mauaji Mwanza Reviewed by on 11:38:00 PM Rating: 5