Mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani (CCM), maarufu kwa jina la ‘Maji Marefu’ amewalipua wabunge waliokosa ubunge katika kipindi hiki na vilivyopita kwa kuhodhi nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mjini Dodoma na kupangisha watu wengine kinyume cha utaratibu wa shirika hilo.
Alisema hali hiyo imefanya wabunge wapya, ambao ni asilimia 70 ya wabunge wote kwa sasa, kukaa nyumba za kulala wageni wakati zipo nyumba hizo kwa wabunge kulingana na mkataba na NHC.
Mbunge alisema wapo watu wamepangishwa na wabunge hao wa zamani, ambao wamegeuza nyumba hizo kama kitega uchumi kinyume na taratibu.
Ngonyani alisema hayo bungeni mjini hapa jana wakati akichangia mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Alimuomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kufuatilia suala hilo na shirika kwa ujumla, aondoe wapangaji hao waliowapangishia wengine kinyume cha utaratibu na kuwapatia nyumba wabunge wapya ambao hawana nyumba za kuishi.
Alisema wabunge hao waliokosa nafasi ya kurudi jimboni miaka tofauti, mkataba wao wa kupangishwa nyumba hizo umekwisha, kwani ukishakosa ubunge hauna dhamana tena mpaka utakaporudi.
“ Kuna wapangaji wengi ambao ni wabunge waliokosa nafasi hiyo ambao wamepangishwa na shirika na badala yake hadi leo wamezishikilia nyumba hizo hawataki kuziachia, ”alisema Ngonyani.
Alieleza kuwa baada ya kukosa nafasi za ubunge na kushindwa kurudi bungeni, wabunge hao walipaswa kurejesha nyumba hizo kwa shirika, ambalo ndilo lenye mamlaka ya kupangisha na si wao kupangisha wapangaji wengine kupitia mikataba yao.
Hata hivyo, taarifa kutoka NHC, Dar es Salaam jana kuhusu nyumba hizo zilifafanua kuwa hazikutengwa kwa ajili ya wabunge pekee, bali hata watu wa kawaida na kila mtu anaingia mkataba binafsi na shirika.
Pia zilieleza kuwa, nyumba hizo zilikodishwa awali kutokana na mahitaji ya wabunge uliokuwapo na wapo walionunua, hivyo wana dhamana nazo.
Aidha ilieleza kuwa ikiwa kuna mpangaji aliyepangisha mtu mwingine bila kujali alikuwa mbunge au la, anakwenda kinyume cha utaratibu, watafuatilia suala hilo.
Katika hatua nyingine, Ngonyani alisema bungeni kuwa NHC imebadilisha dhana na kutoka kwenye kujenga nyumba za bei nafuu, kusaidia wananchi wenye uwezo mdogo sasa inafanya biashara, kwani inajiendesha kibiashara na si kwa lengo la kuundwa kwake.
Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulya (CUF) alisema nyumba za shirika hilo zimejengwa kwa ajili ya mabepari kwa sababu wananchi wa kawaida kutozimudu kutokana na bei zake za kati ya Sh milioni 40 hadi milioni 60.
Mbunge wa Mpanda Vijijini, Moshi Kakoso (CCM) alitaka shirika lijenge nyumba kulingana na uwezo wa watu wa eneo husika kutokana na kuwa wanajenga nyumba za gharama kubwa.
Alisema ujenzi huo uzingatie katika miji inayokua kuiweka katika mandhari nzuri na wakazi wa maeneo husika kumudu kupanga na kununua.
Waliokosa Ubunge Walipuliwa Bungeni, Mbunge Adai NHC Imepoteza Mwelekeo
Reviewed by
on
10:16:00 PM
Rating: