WAZIRI Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye amezitaka nchi za Afrika kuhakikisha zinakubali kubadilishana madaraka pale chama kimoja kinaposhindwa kuongoza ili kuepusha nchi kuingia kwenye machafuko.
Aidha, Sumaye alisema ni vyema wataalam wakaongoza nchi kwa kubuni mbinu mbalimbali za kujikwamua kiuchumi.
Sumaye aliyasema hayo jana Jijini hapa wakati akizungumza kwenye kongamano la Nafasi ya Wasomi na Wafanyabiashara Katika Kujenga na Kukuza Uchumi wa Nchi, lililoshorikisha viongozi wa vyama, wafanyabiashara na wasomi wa kada mbalimbali wa Arusha.
Sumaye alisema uongozi ni kubadilishana nafasi na katika nchi za Ulaya kwa mfano, chama kikishindwa kutawala kinakubali lakini kwa nchi za Afrika kuna uroho wa madaraka au ubinafsi.
"Tunataka kuwajengea uwezo wasomi wetu kwa kujiamini na kujipatia fursa za kujikwamua kiuchumi," alisema Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 mfululizo kati ya 1995-2005, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi.
"Ubinafsi tuache, tukishindwa uchaguzi achia ngazi.Mimi niliyasema haya nikiwa CCM na leo hii nipo Chadema nasema unapoang'angania madaraka, aidha unaogopa ukiachia utasababisha machafuko au ubinafsi."
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Dk. Vincent Mashinji akifungua kongamano hilo, alisema chama chake kinataka kutengeneza mabepari wa kitanzania ambao watajiongeza wenyewe katika kujiinua kiuchumi.
Alisema Arusha ni mji wa kitalii hivyo ni vyema wafanyabiashara wakatumia fursa zilizopo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi, na inawezekana Jiji hilo kuwa na fursa nyingine za kibiashara badala ya kutegemea madini ya Tanzanite pekee.
Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye Akerwa na Ving'ang'anizi wa Madaraka
Reviewed by
on
12:14:00 PM
Rating: