Majambazi Yaliyotoroka Mapangoni Jijini Mwanza Yazua Hofu......Baadhi ya Wananchi Waanza Kuyahama Makazi Yao
Siku moja baada ya kutokea
mapambano ya zaidi ya saa 16 baina ya Jeshi la Polisi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi
kwenye mapango ya mlima ya Utemini, wananchi wa eneo hilo wameingiwa na hofu ya
usalama wao baada ya baadhi yao kuona wahalifu wakitoroka wakati wa tukio hilo.
Wananchi hao wana hofu kuwa majambazi
waliotoroka wanaweza kurejea na kuwadhuru na tayari baadhi wameanza kuhama
makazi yao.
Hofu ya wananchi hao imekuja
baada ya polisi kupambana na watu hao usiku wa kuamkia juzi, wakitumia silaha
kali zilizo sababisha kizaazaa kwa wakazi wa Utemini, kutokana na milio ya
risasi na mabomu.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Utemini
Ibanda, kata ya Mkolani, Jukael Kiula jana alisema baadhi ya wananchi
wanaoishi jirani na mapango hayo wameanza kuhama makazi yao wakihofia kurejea
kwa majambazi hao.
“Kwa mujibu wa maelezo ya
baadhi ya majirani, walikuwa wakiwaona watu wakipanda na kushuka kutoka kwenye
milima yenye mapango waliyojificha watu hao. Lakini hawakuwatilia shaka
wakidhani ni watu wanaopasua mawe, hadi siku polisi walipopambana na majambazi
hayo,” alisema Kiula.
Mwenyekiti huyo aliiomba
Serikali kuimarisha ulinzi na doria kwenye mtaa huo ili kuwahakikishia usalama
wananchi.
“Hata ikibidi, askari wa Jeshi
la Wananchi waweke kambi ya muda kwenye eneo hilo kudhibiti vitendo vyovyote
vya uvamizi,”alisema.
Akizungumza na wakazi wa
Utemini jana, mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga aliwahakikishia kuwa
Serikali itaimarisha ulinzi kudhibiti uwezekano wa wahalifu kuendelea kutumia
mapango hayo kujificha.
Konisaga ambaye alitembelea
eneo la tukio jana, aliwaomba wakazi kutoa taarifa za maficho ya wahalifu pale
wanapohisi kuna nyendo zinazotilia shaka.
Kamanda wa polisi wa Mwanza,
Ahmed Msangi alisema kiama cha wahalifu kimefika na kwamba tayari vyombo vya
dola vimebaini mitandao ya uhalifu na wahusika na itawasaka usiku na mchana.
“Hatutakuwa na msalie mtume
katika mapambano dhidi ya ujambazi Mwanza. Wote wanaojihusha na ujambazi
watambue kuwa yatawakuta yaliyowakuta wenzao waliojaribu kupambana na polisi,”alionya Kamanda Msangi.
Mkuu wa Mkoa, John Mongella
alisema mkakati wa kuifanya Mwanzaa iwe salama umeanza na hakuna mhalifu
atakayeingia Mwanza na kutoka salama.
Majambazi Yaliyotoroka Mapangoni Jijini Mwanza Yazua Hofu......Baadhi ya Wananchi Waanza Kuyahama Makazi Yao
Reviewed by
on
10:49:00 PM
Rating:
