Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kitawashtaki Mahakama ya Kimataifa (ICC) viongozi wa Serikali ambao walitumia mamlaka yao vibaya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, wakiwamo Waziri wa Mambo ya Ndani na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu.
CUF, chama kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar kinachodai kuwa mgombea wake wa urais alishinda kwenye uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, 2015, kimesema kwa sasa kinatumia kampuni mbili za kisheria, moja ya ndani na nyingine ya nje, kuwasaidia katika kushughulikia suala hilo.
Mbali na vigogo hao wawili wa Serikali, chama hicho kimesema hatua hiyo pia itawahusisha viongozi na watumishi wa umma ambao hawakuchukua hatua kwa dhuluma iliyofanywa kwa Wazanzibari wakati na baada ya uchaguzi.
CUF imesema hatua hiyo itachukuliwa baada ya jana kuzindua ripoti yake ya uvunjwaji wa haki za binadamu visiwani humo wakati wa uchaguzi huo.
Mbali na kuwafikisha ICC, Mazrui alisema tayari chama hicho kimeanza kuchukua hatua stahiki ili kuwafikisha viongozi hao kwanza mbele ya Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kutochukua hatua dhidi ya uovu uliokuwa unafanywa Zanzibar wakati wa kipindi hicho.
Iwapo CUF itatekeleza azima hiyo, itakuwa tukio la kwanza kwa Tanzania kupeleka viongozi wake kwenye mahakama hiyo inayopingwa na viongozi wa Afrika wanaodai kuwa wana vyombo vyao vya kushughulikia haki za binadamu.
Tayari viongozi wawili wa Kenya, Rais na makamu wake wameshafikishwa kwenye mahakama hiyo, lakini kesi dhidi yao ilikosa nguvu baada ya mashahidi kukataa kwenda kutoa ushahidi.
Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Salim Jecha Salim alifuta matokeo ya urais, wawakilishi na madiwani Oktoba 28, mwaka jana siku ambayo alitakiwa atangaze mshindi wa mbio za urais.
Alifuta wakati matokeo ya majimbo 31 kati ya 40 yameshatangazwa na kubakia majimbo tisa ambayo matokeo yalishabandikwa vituoni.
CUF ilidai kuwa ilishinda na Jecha alipotangaza uchaguzi wa marudio, chama hicho kilijitoa na hivyo CCM kushinda viti vyote.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Naibu katibu mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema chama chake kinakamilisha ripoti ya ukiukwaji wa wa haki za binadamu uliofanywa wakati wa mchakato huo ambao chama hicho kina ushahidi wa kutosha.
Alisema ripoti hiyo ina matukio yote yaliyotokea kuanzia uandikishaji, kampeni, kuahirishwa kwa uchaguzi na hata kurudiwa.
“Hakuna mtu aliyechukuliwa hatua za kisheria ili kutenda haki kwa waathirika,” alisema akizungumzia vitendo vya wananchi kupigwa na askari, kurushiwa risasi za moto, kubambikiwa kesi, mashambulizi yaliyofanywa na mazombi na uchomaji nyumba za wafuasi na ofisi za wafuasi wa chama.
Shaweji Mketo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF alifafanua kuwa licha ya viongozi hao wa wizara na Jeshi la Polisi kuanza kushtakiwa kwenye mahakama za ndani, ICC itawahusisha watu wengi zaidi.
Alisema juhudi za makusudi zimechukuliwa na chama hicho kuwatafuta washauri wa masuala ya kisheria na uendeshaji wa ICC ili kukusanya ushahidi wa kutosha utakaowatia hatiani wahusika wote.
“Waziri, IGP na baadhi ya askari watahusika. Tunayo majina yao na uchunguzi wetu utakapokamilika tutawataja,” alisema Mketo.
Kuhusu waziri atakayehusika kwenye mashtaka yatakayofunguliwa ICC endapo vigezo vitatosha ni wale waliokuwa kwenye nafasi hiyo wakati hayo yakitokea.
“Zipo kampuni mbili zinatushauri na kutusaidia kukusanya ushahidi,”alisema bila kuzitaja, lakini akafafanua kuwa moja ni ya nje na nyingine ya ndani.
Alisema hazitaji majina kwa kuwa Serikali inaweza ikaingilia kati na kukwamisha mchakato mzima.
Baada ya uzinduzi wa ripoti hiyo uliofanyika jana, Mazrui alisema wamepanga kumuandikia barua Rais John Magufuli na kumkabidhi nakala kwa kuwa ni Amiri Jeshi Mkuu, ajue kinachoendelea ndani ya utawala wake.
Alisema ripoti hiyo pia itapelekwa kwenye jumuiya, taasisi na mashirika ya kimataifa yanayotetea haki za binadamu ulimwenguni.
Alisema CUF imebaini mipango ya Serikali ya kutaka kuwakamata viongozi wake wa Zanzibar na “kuwaweka kwenye magereza ya Bara ili kuwanyamazisha Wazanzibar”.
Ili kuongeza uwazi kwa wanaharakati wa ndani, alisema ripoti ya chama chake sambamba na vielelezo vyote muhimu, itapelekwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) na taasisi nyingine zinazojishughulisha na masuala ya haki za binadamu nchini.
Ili kuongeza uwajibikaji, alisema jopo la mawakili wa chama chake linashirikiana na wanasheria wabobezi wa kimataifa ili kukamilisha taratibu zitakazowezesha kuchukuliwa hatua kwa watu wote ambao walichochea au walitoa maagizo yaliyosababisha makosa dhidi ya binadamu.
“Tumeshamuandikia barua IGP na waziri. Hiyo ni moja ya hatua muhimu kabla hujawashtaki,” alisema.
Waziri hakupatikana kuthibitisha kupokea barua hiyo. IGP alisema hajaipata ripoti hiyo, hivyo hawezi kusema chochote juu ya madai yaliyosemwa na CUF. “Nikiipata nitaijibu,” alisema kwa kifupi.
Naibu katibu mkuu wa CCM-Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema hujuma ni sehemu ya siasa za kila siku visiwani humo.
Alibainisha kuwa chama chake ambacho kimekuwa kikitangazwa mshindi tangu siasa za ushindani ziliporejeshwa mwaka 1992, kimekuwa kikihujumiwa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi na kutoa rai kwa CUF kuchukua hatua kama ina uthibitisho.
“Makosa yote ya jinai yanashughulikiwa na vyombo vya dola. Kinachohitajika ni ushahidi wa kutosha,” alisema Vuai.
Pia alitahadharisha dhidi ya siasa za chuki ambazo alisema zinaenezwa visiwani humo licha ya kuwa pazia la Uchaguzi Mkuu limeshafungwa.“Wapo viongozi wanaenda misikitini kuhubiri uongo… hii si sawa,”alisema.
Kuhusu hatua za zinazotarajiwa kuchukuliwa na CUF alisema viongozi wa chama hicho wanajua kuwa wamekosea, hivyo wanajaribu kutafuta namna ya kuwatuliza wanachama wao hasa wale waliopoteza nafasi zao za uwakilishi kwenye Baraza la Wawakilishi.
“Viongozi wanahangaika. Jinamizi la kususia uchaguzi bado linawaandama. Hawaeleweki na ndiyo maana wanajaribu kote kote, Mahakamani na misikitini. Huko ni kutapatapa,” alisisitiza Vuai.
CUF Waishitaki Serikali Mahakama ya Kimataifa (ICC)
Reviewed by
on
3:11:00 AM
Rating: