Happy Birthday Lady Jaydee: Yafahamu maisha yake ya utoto hadi kuja kuwa staa

Lady Jaydee alizaliwa tarehe kama ya leo. Katika kusherehekea siku yake ya kuzaliwa, tunakupa fursa ya kumfahamu zaidi muimbaji huyo nguli kuanzia enzi zake za utoto hadi amekuja kuwa muimbaji mahiri barani Afrika akiwa na album sita hadi sasa.
May mwaka jana nilikutana naye kwa mara ya kwanza na kumfanyia interview ndefu.

“Sisi kwetu tumezaliwa watoto kumi,” alisema Jaydee. “Lakini bahati mbaya watatu wamefariki na tumebakia saba. Familia yetu ni familia ya dini, tumezaliwa kwenye maadili ya kisabato, tumekulia kanisani na nidhamu.”
“Nilikuwa naimba kwaya kanisani, nilishiriki pia kwenye vikundi vya Pathfinder kanisani kwetu tangu nina miaka saba yaani nilikuwa naweza nikasimama mbele ya kanisa nikaongoza watu, nikaimbisha watu wakaimba. Unajua ukiwa mdogo huwezi ukajua kama ni kipaji, mimi nikawa naona ni kitu tu ambacho napenda, kwahiyo nikawa nafanya tu for fun.”
Jaydee anasema alikuwa ni mtoto msikivu na aliyekuwa akifuata kile alichokuwa akielekezwa na wakubwa zake. “Muda mwingi nilikuwa nautumia kanisani zaidi, kwahiyo ilikuwa ni shule, kanisani,” anakumbuka.
Anasema tangu alipojitambua, muziki kilikuwa ni kitu alichopenda kuja kukifanya kama kazi yake.
“Nilikuwa napenda kuwaangalia watu ambao wanaimba na kujiweka kwenye viatu vyao na kujifikiria vipi mimi nikiwa kama yule, sikuwa najiona mtu mwingine zaidi ya mwanamuziki.”
Lady Jaydee alizaliwa mkoani Shinyanga hadi darasa la nne kabla ya kuhamia jijini Dar es Salaam. Akiwa Dar es Salaam, pamoja na kuwa na ndoto ya kuja kuwa mwanamuziki, alijikuta katika wakati mmoja akifanya kazi kama mtangazaji wa redio.

“Saa zingine nilikuwa najaribu kutangaza TV kwahiyo nakaa kwenye kioo najiangalia najaribu kuona kama naweza kuwa presenter. Kwahivyo nikasema ngoja nikajaribu kuomba labda kwenye redio pia nione kama ntaweza, lakini mwenyewe binafsi siamini kama ni mtangazaji. Ila nafikiri nilikuwa naenda kwasababu napenda muziki na naona ndio sehemu ambayo naweza nikakutana na watu ambao tunaweza tukafanya masuala hayo ya muziki na vitu kama hivyo.”
“Nilifanya ile kazi lakini sio kwamba nilikuwa naipenda sana kwasababu sio passion yangu. Baadaye nilipoweza kufanya muziki nikaona siwezi kuendelea na kitu ambacho hakipo kwenye moyo wangu, nikaona nifanye muziki na niache kutangaza.”
Wimbo wa kwanza Lady Jaydee kurekodi uliitwa ‘Sema Unachotaka’ aliourekodi kwenye studio za Master J baada ya kushinda shindano lililoandaliwa na Radio One Stereo. Wimbo huo uliwekwa kwenye album iitwayo Asubuhi iliyokuwa na nyimbo za wasanii wengine pia. Album yake ya kwanza ilikuwa ni Machozi iliyokuwa na nyimbo nyingi za huzuni na kuumizwa japo anasema hiyo haikuashiria kuwa hayo ndio yalikuwa maisha yake.
Kabla ya kuwa na jina, Jaydee alikuwa akirap na Dr. Dre ambaye hadi leo ni role model wake, alikuwa mmoja wasanii aliokuwa akiwasikiliza sana. Ndoto yake hadi leo ni kuja kurekodi na producer huyo.
“Siku zote tu nimekuwa nikiwish tu kwamba labda kama angeweza kunitengenezea hata wimbo mmoja,” anasema Jaydee.
Maisha ya umaarufu yamekuwa na changamoto nyingi kwake ikiwemo kujizuia kufanya mambo anayoyapenda ambayo kama asingekuwa staa angeyafurahia kuyafanya. “Watu wanashindwa kuelewa kwamba mimi ni Jaydee sawa lakini mimi ni Judith na ni binadamu wa kawaida.” anasisitiza.
“Naweza kukasirika, naweza kucheka, naweza kulia, naumia kama mtu mwingine anavyoumia. Lakini wao wanavyochukulia ni kwamba unavyokuwa pale wanapokuwa wameshakufahamu, hutakiwi vitu vingine kufanya kwahiyo unakuwa saa zingine hauko huru sana. Labda mtu amekuja amekuchokoza inabidi umwache tu hauwezi kumrudishia wakati katika hali ya kawaida mtu yeyote anaweza kufight back. Na mimi ni mgomvi sana na huwa sipendi kuonewa, saa zingine unaweza kukuta mtu akakufanyia kitu lakini ukakaa tu kimya, huyo sio mimi lakini inabidi tu nifanye hivyo.”
Happy Birthday Lady Jaydee.
Happy Birthday Lady Jaydee: Yafahamu maisha yake ya utoto hadi kuja kuwa staa Happy Birthday Lady Jaydee: Yafahamu maisha yake ya utoto hadi kuja kuwa staa Reviewed by on 4:28:00 AM Rating: 5